Utafiti wa Matumizi ya Tumbaku kwa Watu Wazima
Utafiti wa Matumizi ya bidhaa za tumbaku kwa Watu wazima ulitekelezwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali – Zanzibar (OCGS-Zanzibar) kwa kushirikiana na Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (MoHCDGEC) na Wizara ya Afya Zanzibar (MOHZ). Msaada wa kiufundi ulitolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), CDC, na RTI International. Msaada wa kifedha ulitolewa na CDC Foundation kwa msaada kutoka kwa Bill & Melinda Gates Foundations.
Lengo kuu la utafiti ilikuwa kutoa takwimu za matumizi ya bidhaa za tumbaku kwa watu wazima kitaifa na umhimu wa udhibiti wa matumizi ambao unaweza ukalinganishwa na nchi zingine zinazotoa viashiria vya matumizi ya bidhaa za tumbaku na jitihada za kudhibiti matumizi.
Matumizi ya tumbaku ni moja ya sababu inayomweka mtu kwenye hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza (NCDs). Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa kwa mwaka 2010 magonjwa yasiyo ambukizwa (NCDs) yalichangian vifo kwa asilimia 27 ya vifo vyote vilivyotokea. Mwaka 2008, magonjwa yasiyoambukiza (NCD) yalisababisha jumla ya vifo 75.7 na 58.8 kwa kila watu 1,000, ambapo 42.8% walikuwa wanaume na 28.5% walikuwa wanawake chini ya umri wa miaka 60.
Matumizi ya tumbaku ni kichocheo kinachopelekea kupata aina kuu nne za Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCDs) - saratani, ugonjwa mfumo wa damu, ugonjwa sugu wa mfumo wa hewa, na kisukari. Ni sababu kuu inayozuilika isababishayo vifo vya mapema na magonjwa duniani kote na huua zaidi ya watu milioni 7 kila mwaka. Zaidi ya vifo milioni 6 kati ya hivyo vinatokana na matumizi ya moja kwa moja ya tumbaku, huku takribani 890,000 vikiwa ni matokeo ya watu wasiovuta sigara kuathirika na moshi wa watumiaji wa bidhaa za tumbaku (SHS). Mfumo thabiti wa ufuatiliaji wa ufanisi ni muhimu kufuatilia matumizi ya tumbaku na kutathmini afua za kuzuia na kudhibiti matumizi ya tumbaku. wa mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2014 zinaweka msingi wa Sera ya Kudhibiti matumizi ya Tumbaku.