SG Dkt. Msengwa: NBS Itahakikisha Takwimu Rasmi Zinazozalishwa kwa Ubora Kusaidia Mipango ya Maendeleo
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo itahakikisha Takwimu rasmi zinazozalishwa, zinatumiwa ipasavyo na watunga sera pamoja na wadau wa Takwimu katika kupanga mipango endelevu kwa maendeleo ya Wananchi.
Dkt. Msengwa ameyasema hayo wakati akifungua Mdahalo wa Kisera kuhusu Ripoti za Kina za Uhamiaji na Ukuaji wa Miji, Mienendo ya Idadi ya Watu na Maendeleo pamoja na Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Morena jijini Dodoma tarehe 21 Julai 2026.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kushuhudia ongezeko la idadi ya watu linalochangiwa na viwango vya juu vya uzazi pamoja na idadi kubwa ya vijana ambapo hali hiyo inaleta fursa ya kuwa na nguvu kazi kubwa, lakini pia inaongeza shinikizo katika kuboresha huduma muhimu za jamii kama elimu, afya na maji kutokana na ongezeko la watu linalotarajiwa kufikia milioni 115 mwaka 2050.
“Machapisho haya matatu yanaonesha wazi kuwa masuala ya ongezeko la watu, uhamaji, maendeleo ya miji na uhifadhi wa mazingira hayawezi kushughulikiwa kila moja kivyake, bali yanahitaji mipango jumuishi na utekelezaji wa sera unaoratibiwa kwa pamoja,” Amesema Dkt. Msengwa.
Hivyo, Ameeleza kuwa mdahalo huo unafanyika katika kipindi muhimu ambapo Tanzania inaendelea kutekeleza agenda yake ya maendeleo pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan yale yanayohusu miji endelevu, hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na maendeleo jumuishi.
Amesema mapendekezo yatakayotokana na mdahalo huo yataimarisha sera za kitaifa na kisekta, kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali, huku yakihamasisha matumizi makubwa ya Takwimu rasmi katika kupanga, kufuatilia na kutathmini maendeleo.
Aidha, Dkt. Msengwa ametoa shukrani zake dhati kwa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji – IOM, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi - UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto - UNICEF, Benki ya Dunia, UN Women, USAID, FCDO, Ofisi ya Sensa ya Marekani, Serikali ya Jamhuri ya Korea, Jamhuri ya Watu wa China pamoja na wadau wengine.