Cosmas: NBS Inaendelea, Utafiti Sekta ya Biashara kwa Awamu ya Pili
Meneja wa Takwimu za Mazingira na Makazi Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, Stephano Cosmas amesema Ofisi hiyo inaendelea na awamu ya pili ya Utafiti wa Fedha katika Biashara Ndogo na za Kati, lengo likiwa ni kuboresha takwimu za sekta hiyo muhimu ya uchumi.
Cosmas ameyasema hayo wakati wa mahojiano katika Kipindi cha Jambo Tanzania cha Shirika la Utangazaji Tanzania – TBC1 jijini Dodoma tarehe 16 Machi 2026.
Cosmos amesema awamu ya kwanza ya Utafiti huo ilifanyika mwaka 2010, na matokeo yake yalikuwa chini ya matarajio, hali iliyochochea kuanzishwa kwa awamu ya pili ili kupata takwimu sahihi zaidi kuhusu mwenendo wa kifedha wa biashara ndogo na za kati.
Ameongeza kuwa utafiti huo unaofanywa kwa ushirikiano na wafanyabiashara wa ngazi mbalimbali, unatarajiwa kusaidia kubaini vifurushi maalumu vya kifedha vitakavyokuza biashara hizo, huku akisisitiza kuwa tafiti hizo zina mchango mkubwa katika kupima maendeleo ya sekta hiyo na mwelekeo wake wa baadaye.
Aidha, mahojiano hayo yamefanyika ikiwa ni siku saba (7) zimepita tangu Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, atangaze kupitia Mkutano wake na vyombo vya habari kuanza kwa tafiti hizo nne muhimu za kitaifa zitakazokusanya taarifa za kina kuhusu shughuli za biashara, sekta isiyo rasmi, huduma za fedha kwa wafanyabiashara wadogo na uzalishaji viwandani, hatua inayolenga kuimarisha mipango ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
Kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura ya 351, Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS imepewa jukumu la kuratibu na kusimamia uzalishaji, uchakataji na usambazaji wa takwimu rasmi nchini.
Tafiti hizo ambazo tayari zimeshaanza ni Utafiti wa Kina wa Shughuli za Kibiashara, Utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi, Utafiti wa Huduma za Fedha kwa Wafanyabiashara Wadogo Sana, Wadogo na wa Kati – FINSCOPE MSMEs pamoja na Utafiti wa Uzalishaji Viwandani ambazo taarifa zake ndizo zitakazokusanywa uwandani.
Madhumuni ya tafiti hizo ni kukusanya taarifa muhimu kuhusu shughuli za biashara katika sekta rasmi na zisizo rasmi, ikiwemo uzalishaji viwandani, ajira, uwekezaji na mazingira ya biashara nchini ambapo amesema taarifa zitakazopatikana zitaisaidia Serikali pamoja na wadau wa sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na watafiti kubuni programu mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Tafiti hizo zitasaidia kuhuisha takwimu za thamani ya pato ghafi ambalo linaendana na uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali, kwa lengo la kubaini mchango wa shughuli hizo za kiuchumi katika Pato la Taifa.