The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Dkt. Chuwa Atoa Mafunzo ya Maadili ya Takwimu kwa Watumishi Wapya NBS
Posted On: 21 February, 2026
Dkt. Chuwa Atoa Mafunzo ya Maadili ya Takwimu kwa Watumishi Wapya NBS

Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mstaafu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Maadili ya - ISI Dkt. Albina Andrew Chuwa, amewaasa watumishi wapya wa umma kuzingatia maadili, uadilifu na weledi katika matumizi ya takwimu, akisisitiza kuwa takwimu zenye kuzingatia maadili ni msingi wa maendeleo ya taifa na kujenga imani ya umma.

Akizungumza katika
mafunzo hayo yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ngorongoro, Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS jijini Dodoma, Dkt. Chuwa amesema takwimu rasmi zina mchango mkubwa katika kupanga sera, kugawa rasilimali na kuongoza utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya muda mrefu ya nchi.

Dkt. Chuwa amesisitiza kuwa uadilifu katika uzalishaji na matumizi ya takwimu huimarisha uhuru na uaminifu wa matumizi ya Mfumo wa Taifa wa Takwimu, huku akiwahimiza watumishi hao kuwa waaminifu na kuepuka shinikizo linaloweza kuathiri ubora wa takwimu.

Ameongeza kwa kusema,  mafanikio ya Tanzania katika kuimarisha uaminifu wa takwimu rasmi kwa umma kupitia maboresho ya kisheria na kitaasisi, akibainisha kuwa imani ya umma katika takwimu imeongezeka kutoka asilimia 70 kwa mwaka 2014 na kufikia asilimia 79.2  kwa mwaka 2024.

Aidha, ametaja changamoto zinazoikabili taaluma ya takwimu katika nchi zinazoendelea, ikiwemo uhaba wa rasilimali, mapungufu ya mifumo ya kisheria, uelewa mdogo wa takwimu kwa umma pamoja na hatari mpya za ulinzi wa taarifa zinazosababishwa na kukua kwa teknolojia.

Dkt. Chuwa amehitimisha kwa
amewahimiza watumishi hao kuendelea kujifunza, kuzingatia uwajibikaji na kushiriki katika vyama vya kitaaluma kama vile Chama cha Watakwimu Tanzania - TASTA ili kuimarisha maadili ya taaluma ya takwimu nchini na kukusanya takwimu sahihi zitakazosaidia kufikia malengo ajenda ya Umoja wa Afrika ya Mwaka 2063. Kikao hicho kilikuwa sehemu ya programu ya kuwajengea watumishi wapya uwezo wa kusaidia maamuzi yanayotegemea ushahidi na kuimarisha uwazi katika utumishi wa umma.