NBS Accessibility Tools
NBS Accessibility Tools

Text Size

Language

Inflation Rate for July, 2026: 4.2% AASS 2023/2024 Women's Empowerment and Nutrition Module: WEN Tanzania Gender and Environment Survey: TGES 2025 Utafiti wa Kufuatilia Kaya (National Panel Survey, Wave 6: NPS 2026
The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Dkt. Minja Afungua Warsha ya Kitaifa Upatikanaji Takwimu za Kupima Mabadiliko ya Tabianchi
Posted On: 02 September, 2026
Dkt. Minja Afungua Warsha ya Kitaifa Upatikanaji Takwimu za Kupima Mabadiliko ya Tabianchi

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ofisi ya Taifa ya Takwimu -NBS, Dkt. Ruth Minja kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Amina Msengwa, tarehe 01 Septemba 2026 amefungua warsha ya kitaifa ya siku mbili kuhusu upatikanaji wa Takwimu za kupima mabadiliko ya Tabianchi kwa mtazamo wa kijinsia kwa ajili ya kuboresha sera za kukabiliana na kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi nchini.

Akizungumza wakati wa hotuba ya ufunguzi wa warsha hiyo inayofanyika kwenye Ukumbi wa Serengeti uliopo katika Hoteli ya Best Western Dodoma City jijini Dodoma, Dkt. Minja amesema orodha ya Kimataifa ya Takwimu na Viashiria vya Mabadiliko ya Tabianchi, mahitaji ya utoaji wa taarifa chini ya Mkataba wa Paris wa Mwaka 2015, matokeo ya Utafiti wa Jinsia na Mazingira Tanzania wa Mwaka 2025, pamoja na vipaumbele na vyanzo vingine vya takwimu za kitaifa vinaimarisha upatikanaji wa ushahidi wa kitakwimu unaohitajika katika utungaji wa sera, upangaji wa mipango, ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa.

Washiriki wa warsha hiyo ambayo inaratibiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira - UNEP na Idara ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa – UNSD, ni wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Madini na Wizara ya Maji.

Wataalam wengine wanaoshiriki warsha hiyo ni kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Afya, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Tume ya Mipango, Mamlaka ya Hali ya Hewa - TMA, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira - NEMC, Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni – NCMC, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - UDSM, Chuo Kikuu cha Dodoma – UDOM, Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika – EASTC na Mtandao wa Jinsia Tanzania – TGNP.

Dkt. Minja amesema warsha hiyo inalenga kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu upatikanaji, uzalishaji na matumizi ya takwimu za mabadiliko ya tabianchi kwa mtazamo wa kijinsia, pamoja na namna Takwimu hizo zinavyoweza kutumika kuimarisha sera na hatua za kukabiliana na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.

“Warsha hii ni muhimu kwa kuwa mabadiliko ya tabianchi, mazingira na jinsia ni masuala mtambuka yanayohitaji ushirikiano wa karibu wa taasisi na sekta mbalimbali. Hakuna taasisi moja yenye taarifa zote zinazohitajika kuelewa kikamilifu uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi na jinsia.” Amesema Dkt. Minja na kuongeza;

“kuwakutanisha wataalamu kutoka maeneo mbalimbali kutasaidia kujenga uelewa wa pamoja, kuimarisha ubadilishanaji wa takwimu na kuweka msingi wa ushirikiano endelevu kati ya wazalishaji na watumiaji wa takwimu.”

Dkt. Minja amesema kupitia warsha hiyo kutakuwa na majadiliano ambayo yataongeza uelewa kuhusu namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri jamii, shughuli za kujipatia kipato, maliasili na maendeleo ya uchumi, kwa kuwa athari zake hazigusi watu wote kwa kiwango sawa.

Kiongozi huyo amefafanua kuwa wanawake na wanaume mara nyingi hukabiliwa na viwango tofauti vya kuathirika, wana fursa tofauti za vipato, kumiliki na kutumia rasilimali, na hutekeleza majukumu tofauti katika hatua za kukabiliana na kupunguza mabadiliko ya tabianchi. Hivyo, sera madhubuti zinahitaji takwimu sahihi, za kuaminika na zilizochambuliwa kwa kuzingatia jinsia na sifa nyingine za kijamii na kiuchumi.

Maeneo mahususi yatakayojadiliwa ni pamoja na uzalishaji, usimamizi, ujumuishaji, uchambuzi, ubadilishanaji na matumizi ya takwimu za mabadiliko ya tabianchi, mazingira na jinsia. Washiriki watapendekeza hatua za kuimarisha Mfumo wa Taifa wa Takwimu ili kuwezesha uzalishaji endelevu wa takwimu zilizochambuliwa kwa kuzingatia jinsia kwa ajili ya kutunga, kutekeleza na kufuatilia sera na mipango jumuishi ya maendeleo.