Dkt. Msengwa: Takwimu Rasmi ni Msingi Kufikia DIRA 2050
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha ukusanyaji na uchakataji wa taarifa ili kuzalisha Takwimu rasmi, unafanyika kwa ufanisi mkubwa ili kusaidia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Dkt. Msengwa amesema hayo alipokuwa akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, wakati wa hafla ya ufungaji wa mafunzo ya uandaaji wa Wasifu wa Kijamii na Kiuchumi wa mikoa iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma tarehe 14 Mei 2026.
“Tangu Waraka uliotolewa na Waziri Mkuu wa Mwaka 2012 ulioelekeza kuandaa Wasifu za Kiijamii na Kiuchumi za Mikoa, sasa ni kwa mara ya kwanza tunafanya zoezi hili kwa pamoja nchi nzima, hii hatua kubwa sana katika kuimarisha mfumo wa Takwimu nchini,” Amesema Dkt. Msengwa.
Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu, kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura ya 351, ina jukumu la kuratibu ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa takwimu rasmi nchini, huku zoezi hilo likiwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa majukumu hayo.
Aidha, alieleza kuwa mafunzo hayo yanahusisha washiriki 3,098 pamoja na wakufunzi 12 wakisaidiwa na Mameneja wa Takwimu wa Mikoa na wataalamu wengine wa takwimu waliopo katika mikoa yote.
“Tunatumia teknolojia ya mtandao. Mkufunzi mmoja anaweza kufundisha washiriki waliopo Dodoma, Manyara, Iringa na maeneo mengine kwa wakati mmoja. Hii imetupa nafasi ya kujenga uelewa wa pamoja kwa watu zaidi ya 3,000 kwa wakati mmoja,”Amesema Dkt. Msengwa.
Dkt. Msengwa amefafanua kuwa nyenzo zinazotumika katika mafunzo hayo zimeboreshwa ili ziendane na mahitaji ya sasa pamoja na Dira ya Taifa ya 2050, Mpango wa Taifa wa Maendeleo na mipango mingine ya muda mrefu.
“Kila mpango wa maendeleo unahitaji takwimu sahihi. Tunataka kuhakikisha takwimu rasmi zinaendelea kukusanywa kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa,” Amesisitiza Dkt. Msengwa.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo ambayo yamewahusisha watumishi kutoka Halmashauri za Mikoa yote, maafisa wa idara mbalimbali pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na TAMISEMI yatawasaidia wataalamu wa mikoa na halmashauri kuwa na uwezo mkubwa wa kuelezea kwa wananchi masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii kwa kutumia takwimu sahihi.
“Tunapozungumzia mfumuko wa bei au pato la taifa, tunataka wataalamu wetu waweze kumwelewesha mwananchi wa kawaida kwa lugha rahisi kwamba takwimu hizo zina maana gani katika maisha yake ya kila siku,”Amesema Dkt. Msengwa.