Kamati ya Bunge ya Bajeti Yaipongeza Wizara ya Fedha Kuifanya NBS Kuwa Chanzo cha Takwimu Rasmi Nchini
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imetoa pongezi kwa Wizara ya Fedha kwa kuisimamia vema na kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS kuendelea kuzalisha, kuchakata na kusambaza Takwimu rasmi nchini ambazo ni muhimu kwa Serikali na wadau katika kupanga mipango ya maendeleo kwa Wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma tarehe 12 Agosti 2026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Mashimba Ndaki alipokuwa akifunga kikao cha Kamati yake na Watendaji wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Ofisi hiyo Mhe. Anne Semamba Makinda, kilichofanyika kwenye Ukumbi Msekwa B Jengo la Pius Msekwa.
“Mheshimiwa Naibu Waziri, Mwenyekiti wa Bodi ya NBS pamoja na Watumishi wote, kwa niaba ya Wajumbe wote wa Kamati ninawapongeza kwa kazi nzuri na kubwa mnayoifanya…na kipekee tunampongeza Rasmi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Ofisi hii kutekeleza majukumu yake na kufanya tafiti mbalimbali ambapo matokeo ya tafiti hizo yanaisaidia Serikali na wadau katika kupanga mipango inayowaletea Wananchi maendeleo.’’ Amesisitiza Mhe. Ndaki.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ndaki amempongeza Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) aliyeshiriki kikao hicho akimuwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Musa Omar (Mb) kwa taarifa na mawasilisho mazuri nay a kina yaliyofanywa na Wataalam wa NBS.
Mawasilisho yaliyowasilishwa kwa Wajumbe wa Kamati hiyo ni kuhusu Pato la Taifa, Fahirisi za Bei za Taifa, Matokeo ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa Mwaka 2025 pamoja na Matokeo muhimu ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi kwa Mwaka 2025.
Awali akitoa utangulizi kwa Kamati hiyo kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Ruth Minja amesema Ofisi hiyo inatambua wajibu mzito wa kisheria iliyopewa na Serikali wa kuzalisha, kuchakata na kusambaza Takwimu rasmi zenye ushahidi unaokidhi vigezo vya kitaifa na kimataifa, ili ziweze kutumiwa na Serikali pamoja na Wadau kwa ajili ya kupanga mipango ya kuinua Uchumi na kuwaletea maendeleo Wananchi.
Aidha, pamoja na viongozi wengine, kikao hicho kilihudhuliwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb).