The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Karugendo Apongeza Ushirikiano Kati ya NBS, Jeshi la Magereza
Posted On: 06 February, 2026
Karugendo Apongeza Ushirikiano Kati ya NBS, Jeshi la Magereza

Mkurugenzi wa Uratibu, Utafiti na Shughuli za Kitakwimu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, Emilian Karugendo amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Ofisi hiyo na Jeshi la Magereza hususan katika kushauriana na kubadilishana takwimu.

Karugendo ametoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Suleiman Msengwa, wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Utafiti kuhusu Ufanisi wa Programu za Urekebishaji wa Wafungwa yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Rugimbana, Msalato jijini Dodoma tarehe 04 Februari 2026, ambapo Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu.

Mkurugenzi Karugendo amelihakikishia Jeshi hilo kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ipo tayari kutoa Wataalam ambao watashirikiana na Wataalam wa Jeshi hilo ili kupata takwimu sahihi zenye ubora unakidhi viwango vya kitaifa vya ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu kwa ajili ya matumizi ya mipango ya Taifa hususan katika kuboresha huduma za urekebishaji wa wafungwa nchini.

Akifungua rasmi mafunzo hayo ya siku tatu (tarehe 04 hadi 06 februari 2026), Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, amesema kuwa Jeshi hilo limefanya mapitio ya kina ya utaratibu wa awali wa urekebishaji na kuandaa mwongozo mpya unaojikita katika hatua nne muhimu za urekebishaji, ikiwemo hatua ya mapokezi ya wafungwa.

CGP Katungu amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo washiriki wa kufanya utafiti huo ambao utasaidia kupima ufanisi wa programu hizo.

Aidha, CGP Katungu amesema Jeshi la Magereza limeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kama Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi - VETA na Chuo cha Uhasibu Arusha - IAA katika kuibua na kuendeleza ujuzi wa wafungwa kupitia shughuli za uzalishaji na mafunzo ya stadi za kazi.

CGP Katungu ameongeza kuwa hivi karibuni Jeshi la Magereza liliandaa mazingira kwa mahabusu 12 wa Gereza la Babati kufanya Mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2025, ambapo matokeo yalionesha mafanikio makubwa; mahabusu wanne walipata Daraja la Kwanza, mmoja Daraja la Pili, watano Daraja la Tatu na wawili Daraja la Nne. Mafanikio hayo yameelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za kutoa elimu kama nguzo muhimu ya urekebishaji.

Naye Mkuu wa Sehemu ya Utafiti Jeshi la Magereza, DCP Justine Kaziulaya, amewataka washiriki wa mafunzo kusikiliza kwa makini mada zitakazowasilishwa na kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo. Amebainisha kuwa mada zitahusu majukumu ya Jeshi la Magereza, maadili ya utafiti, mbinu za utafiti, ukusanyaji wa takwimu, matumizi ya zana za utafiti na kufanya majaribio ya awali (pre-test) ya dodoso katika magereza jirani.