Mangula Awaapisha Wadadisi wa Utafiti wa FinScope MSMEs
Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS, Oscar Mangula amewaapisha Wadadisi 114 wa Utafiti wa FinScope MSMEs na kuwataka kuzingatia sheria na maadili ya kazi wakati wa ukusanyaji wa taarifa ili kulinda usiri wa taarifa za washiriki wa utafiti huo.
Uapisho huo umefanyika leo tarehe 08 Machi 2026 kwenye Ukumbi wa Amount Uluguru Morogoro mjini, kabla ya mafunzo hayo kufungwa rasmi kesho tarehe 09 Machi 2026 ili zoezi la ukusanyaji wa taarifa za wafanyabiashara wadogo, wadogo sana na wa kati lianze.
Akizungumza wakati wa uapisho huo, Mangula amesema Wadadisi hawapaswi kutumia taarifa watakazokusanya kwa manufaa yao binafsi wala kuzipeleka kwa mtu mwingine ambaye hausiki na Utafiti huo zaidi ya NBS.
Amesema pia sheria inawataka Wadadisi kutekeleza majukumu yao kwa usahihi ndani ya muda na utaratibu uliopangwa na kila kazi ina muda wake ambapo kinyume na hilo ni kosa la jinai huku akisisitiza Wadadisi hao kujikita kuuliza maswali yaliyopo kwenye dodoso pekee na kuepuka kuuliza maswali ambayo hayajaandaliwa kwa matumizi binafsi.
Kadhalika,amewataka Wadadisi kutoomba chochote kutoka kwa Wananchi baada ya kumaliza zoezi la ukusanyaji wa taarifa katika kaya na biashara akieleza kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai ambapo amebainisha kuwa adhabu ya kukiuka sheria hizo ni kifungo cha miezi sita au faini ya shilingi milioni mbili au vyote kwa pamoja.