Masolwa: Takwimu Rasmi Msingi wa Mipango ya Maendeleo Nchini
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, Daniel Masolwa amesema Takwimu rasmi ni msingi na muhimu kwa Serikali na wadau katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo kwa Wananchi kwa kuwa Takwimu zinaonesha kila sekta ina mchango gani kwenye uchumi wa nchini.
Masolwa ameyasema hayo wakati wa mahojiano kwenye Kipindi cha cha “Round About” kinachorushwa na Kituo cha Redio cha C-FM jijini Dodoma mapema leo tarehe 20 Mei 2026.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa Takwimu zinabainisha changamoto na fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwemo za uwekezaji, ajira, masoko na zinginezo, hivyo ameiomba jamii kuwa mstari wa mbele kutumia Takwimu rasmi zinazotolewa na Ofisi hiyo ili kuwekeza katika maeneo sahihi kwa kutumia Takwimu zenye ushahidi.
Kwa upande wake Mtakwimu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Nacky Sinda amesema Takwimu rasmi zinatumika katika kupanga mipango ya maendeleo ikiwemo kwenye sekta ya ajira.
Sinda ametoa mfano wa Utafiti wa Nguvu Kazi (Labour Force) ambao hufanyika kila mwaka kwa lengo la kukusanya viashiria kwa ajili ya uundaji wa sera na programu zinasohusiana na soko la ajira nchini hasa kukuza ajira, kukuza kazi zenye staha pamoja na programu za kuongeza kipato na programu za mafunzo.
“Kwa mfano kupitia Tafiti hizo, Serikali, Wadau pamoja na wawekezaji wanaweza kujua aina za ujuzi uliopo kwenye soko la ajira pamoja na mgawanyo wa nguvu kazi katika maeneo mbalimbali na shughuli za kiuchumi.” Amesema Sinda.
Hivyo, Mtakwimu huyo ametoa rai kwa Wadau na Wananchi kutumia fursa ya uwepo wa Takwimu rasmi katika kupanga mipango yao ya maendeleo na kuondoa dhana ya kwamba Takwimu ni kwa matumizi ya Serikali pekee.