Meserani Juu Yafikiwa Utafiti wa Mifugo
Timu za Wadadisi wa Utafiti wa Kuboresha Njia Bora ya Ukusanyaji wa Taarifa za Mifugo (ng’ombe) pamoja na kiasi cha maziwa kinachozalishwa katika kaya ambazo zinajihusisha na ufugaji wa ng’ombe, zimefika katika Kijiji cha Meserani Juu, Kata ya Meserani, Wilaya ya Monduli, Mkoani Arusha tarehe 01 Aprili 2026.
Utafiti huo ambao utafanyika kwa pamoja kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania – TALIRI kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, una lengo la kuangalia njia bora za kupata idadi ya ng’ombe pamoja na kiasi cha maziwa kinachozalishwa katika kaya ambazo zinajihusisha na ufugaji wa ng’ombe ili kuziba pengo la upatikanaji wa takwimu za kilimo na mifugo nchini.
Tanzania imechaguliwa kuwa ya mfano kati ya nchi 50 duniani ambazo ni mwanachama wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa – FAO ambazo zinashiriki katika Mkakati wa Kuboresha Takwimu za Kilimo ifikapo Mwaka 2030.
Ambapo matokeo ya utafiti huo unaofanyika kwa mikoa ya Arusha na Tabora, yanategemewa kutumika katika nchi hizo ili kuboresha mbinu bora za ukusanyaji wa takwimu za mifugo (ng’ombe) pamoja na mazao yake yakiwemo maziwa.