Mhe. Kwagilwa: Tutunze Mazingira Kuelekea 2050
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa (Mb), amefungua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Mazingira yanayofanyika kwenye viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma leo tarehe 1 Juni 2026.
Akizungumza katika ufunguzi wa maadhimisho hayo Mhe. Kwagila amesema Takwimu zinaonesha ifikapo Mwaka 2050 Tanzania inakadiriwa kuwa na watu takriban Milioni 118 hivyo ni vyema kama Nchi kuweka juhudi katika kutunza mazingira ili kuwezesha mazingira yetu kuendelea kuwa rafiki na kuja kumudu shughuli zote na idadi ya watu hao ifikapo mwaka 2050.
“Ikiwa leo tupo watanzania millioni 61 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, jiulize wewe na mwenzako itakuwaje Tanzania ya miaka 25 ijayo ambayo itakuwa na watanzania milioni 118 kwenye mazingira haya haya. Je, Nini ambacho tunahitaji kufanya? Kwa hakika tunapaswa kuyalinda mazingira kwa wivu mkubwa.” Amesema Mhe. Kwagilwa.
Aidha, katika maonesho ya maadhimisho ya Wiki ya Mazingira, Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea kutumia fursa hiyo kuhakikisha umma na wadau mbalimbali wa Takwimu wanapata Takwimu rasmi za mazingira zenye ushahidi ili kuwawezesha katika kutunga sera na kupanga mipango endelevu kwa ajili ya kuendelea kutunza mazingira.
Maonesho hayo yameanza leo tarehe 01 juni 2026 na kufunguliwa rasmi na Naibu Waziri huyo, huku yakitarajiwa kuhitimishwa tarehe 05 Juni 2026 ambapo Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na Kaulimbiu isemayo: "Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania."