The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Mhe. Makinda Afunga Mafunzo ya Wadadisi, Kuzindua Utafiti ya Finscope MSMEs 2025/2026
Posted On: 14 March, 2026
Mhe. Makinda Afunga Mafunzo ya Wadadisi, Kuzindua Utafiti ya Finscope MSMEs 2025/2026

Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu -NBS, Mhe. Anne Semamba Makinda amefunga rasmi mafunzo ya Wadadisi na Wasimamizi pamoja na kuzindua zoezi la ukusanyaji wa taarifa za Utafiti wa Huduma za Fedha kwa Biashara ndogo sana, ndogo na za kati wa mwaka 2025/2026 (FinScope MSME Survey) halfa ambayo imefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mount Uluguru Hotel, Morogoro mjini tarehe hivi karibuni.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mhe. Makinda amesema kuwa Utafiti huo una umuhimu wa kipekee kwani utasaidia kupata taarifa zinazohusu huduma ya fedha kwa wafanyabiashara wadogo ili kujenga msingi wa kitakwimu utakaosaidia Sera, Mipango na maamuzi mbalimbali yanayohusu huduma ya fedha kwa biashara ndogo.

Mhe. Makinda ameongeza kuwa Utafiti huo ni wa pili kufanyika nchini kwani kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2010 ambapo kwa kipindi chote hicho mambo mengi yamefanyika katika kuboresha upatikanaji wa huduma zinazohusiana na masuala ya fedha hapa nchini. Hivyo, amesema kufanyika kwa Utafiti huo ambao haujafanyika kwa miaka takribani 15 ni jambo la kujipongeza kwa wadau wote wanaohusika kwani umuhimu wake hautiliwi shaka kutokana na asilimia kubwa ya wafanyabiashara nchini Tanzania kuwa ni wafanyabiashara wadogo.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa Wafanyabiashara wadogo sana, wadogo na wa kati wamekuwa miongoni mwa makundi muhimu ambayo yanakumbana na changamoto mbalimbali za kukosa huduma za fedha kutokana na kukosa dhamana na masharti mengine yaliyowekwa na taasisi za fedha.

Aidha, amesema kukosekana kwa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kumepelekea biashara hizo kudumaa hivyo, kutochangia uchumi wa familia na taifa kwa ujumla. Taarifa zitakazopatikana kutokana na Utafiti huo zitasaidia sana watoa huduma za fedha kuboresha mazingira na huduma wanazozitoa ambazo zitasaidia wajasiriamali wadogo na wa kati kuweza kupata huduma bora za fedha. Hili linaweza kufanyika kwa kuanzisha vifurushi maalum kwa makundi tofauti ya wafanyabiashara badala ya kuwachukulia sawa wafanyabiashara wote.

Makinda ameipongeza, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar pamoja na Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania -FSDT kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo ni muhimu katika nchi  ambayo kwa asilimia kubwa Uchumi wa wananchi wake unachangiwa na biashara ndogo ndogo.

Aidha, amewakumbusha na kuwaasa wadadisi baada ya kukamilika mafunzo  kutambua dhamana kubwa waliyopewa na Serikali kuwa watatumia juhudi na maarifa kufanikisha zoezi la ukusanyaji wa taarifa za Utafiti kwa ufanisi.

“Ikumbukwe kwamba kipimo cha mafanikio ya kazi yenu kitaonekana dhahiri wakati wa utoaji wa matokeo ya Utafiti huu. Hivyo, niendelee kuwakumbusha na kuwaasa mzingatie taratibu za utumishi wa umma na kufanya kazi kwa bidii na ufanisi mkubwa.”Amesema Makinda.

Kadhalika, anmewaomba wafanyabiashara watakaofikiwa na wadadisi kushiriki kikamilifu katika utafiti huo kwa kutoa taarifa sahihi ili kusaidia kufanikisha malengo yaliyo kusudiwa na kuiwezesha Serikali kupanga mipango bora ya maendeleo kwa kutumia takwimu bora zenye ushahidi.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema Utafiti huo utafanyika kwa kutumia njia ya teknolojia ya kidigitali ambayo itapunguza gharama za kuchapisha, kusafirisha na kuingiza takwimu kwenye Matumizi ya teknolojia yataboresha ubora wa takwimu zitakazokusanywa na kuwezesha matokeo ya Utafiti kupatikana kwa haraka.  

Pia, Dkt. Msengwa ameongeza kuwa Utafiti huo utafanyika nchi nzima katika mikoa 31 ya Tanzania, ambapo mikoa 26 ni ya Tanzania Bara na mikoa mitano (5) ni ya Zanzibar. Aidha, jumla ya maeneo 815 yamechaguliwa kitaalam kwa ajili ya utafiti huo kati ya hayo, maeneo 695 ni ya Tanzania Bara na maeneo 120 ni ya Zanzibar. Katika maeneo hayo, takriban taasisi za kibiashara 8,150 zinatarajiwa kuhojiwa katika utafiti huu.

Ameongeza kwa kusema kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu -NBS na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar -OCGS ndizo zenye mamlaka ya kukusanya na kutoa takwimu rasmi hivyo zina majukumu ya kuhakikisha kuwa utafiti huu unafanyika kwa viwango na ubora uliokusudiwa. Mbali na hilo, ni jukumu la NBS na OCGS kuhakikisha takwimu hizi mara zitakapokuwa tayari zinasambazwa katika ngazi zote za utawala kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo ya Wananchi. Kazi hii itafanyika mara ripoti ya utafiti huu itakapokuwa tayari na kushirikiana na uongozi wa FSDT kuhakikisha kazi hii inafanyika kama ilivyopangwa.

Aidha, Dkt. Msengwa ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia kufanyika kwa utafiti huo hapa nchini pamoja na Wizara zinazoshikiana kukamilisha Utafiti huo ambazo ni Wizara ya Fedha - Tanzania Bara, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango - POFP Zanzibar, Benki Kuu ya Tanzania - BoT, Wizara ya Viwanda na Biashara – Tanzania Bara, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Wizara ya Kilimo – Tanzania Bara, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar pamoja na Ofisi ya Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha - FSDT na FinMark Trust, kwa kuziamini NBS na OCGS kutekeleza utafiti huo.