The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Mhe. Makinda Ateta, Watumishi Wapya - NBS
Posted On: 21 February, 2026
Mhe. Makinda Ateta, Watumishi Wapya - NBS

Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS, Mhe. Anne Semamba Makinda, amewahimiza watumishi wapya kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo nchini kwani Takwimu zinazotolewa na ofisi ya taifa ya Takwimu hutumika katika kupanga mipango ya maendeleo nchini.

Mhe. Makinda ameyasema hayo tarehe 20 Februari 2026 alipokuwa akitoa mafunzo ya uadilifu na uzalendo kwa watumishi hao ambao wanaendelea na mafunzo mbalimbali, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ngorongoro uliopo katika Jengo la Makao Makuu ya Ofisi hiyo jijini Dodoma.

“Niwaombe, ipendeni sana nchi yenu, fanyeni kazi kwa bidi kwa kuwa Serikali imewaamini na imefanya hivyo kwa sababu mnao uwezo nah ii ni bahati kwenu…nchi hii inao wasomi wengi tena wana uwezo wa kushika nafasi hizo, sasa jiulizeni kwa nini ninyi…maana yake mnao wajibu wa kuitumikia nchi hii kupitia taaluma zenu na nikiwatizama wote ni vijana na mna nguvu ya kutumika, kmatimizeni wajibu wenu.” Amesema Mhe. Makinda.

Mhe. Makinda amehimiza watumishi hao kujenga utamaduni wa kujisomea ili kuendana na kasi ya kukua kwa teknolojia na kuwasisitiza kuwa Sekta ya Takwimu inahitaji ufanisi.

“Niwaambie teknolojia inakuwa kwa kasi sana, na Takwimu zinahitaji ufanisi, jiendelezeni kila wakati ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na uzuri NBS ina fungu hilo hivyo, muda ukifika kasomeni hata kwa njia ya mtandao someni.” Amehimiza Mhe. Makinda.