NBS Accessibility Tools
NBS Accessibility Tools

Text Size

Language

Inflation Rate for July, 2026: 4.2% AASS 2023/2024 Women's Empowerment and Nutrition Module: WEN Tanzania Gender and Environment Survey: TGES 2025 Utafiti wa Kufuatilia Kaya (National Panel Survey, Wave 6: NPS 2026
The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Mhe. Makinda: Teknolojia katika Uzalishaji Takwimu Rasmi Itumike Kutatua Changamoto za Wananchi
Posted On: 24 August, 2026
Mhe. Makinda: Teknolojia katika Uzalishaji Takwimu Rasmi Itumike Kutatua Changamoto za Wananchi

Mwenyekiti wa Bodi ya Usamamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS Mhe. Anne Semamba Makinda amesema ili Serikali iweze kupanga mipango itakayoweza kutatua changamoto zinazowakabili Wananchi, ni vema suala la matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa Takwimu rasmi nchini lizingatiwe na kutumiwa kikamilifu, badala ya Takwimu hizo kubaki kwenye machapisho bila kutumika ipasavyo.

Mhe. Makinda ameyasema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano - MoU kati ya NBS, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - UDSM na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha, Tanzania - NM AIST kwa miaka mitano (2026/2027 hadi 2030/2031), iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Ngorongoro uliopo Jengo la Makao Makuu ya NBS jijini Dodoma tarehe 22 Agosti 2026.

Akisisitiza katika hafla hiyo yenye lengo la kuimarisha matumizi ya teknolojia na akili Bandia katika kuzalisha Takwimu rasmi, Kiongozi huyo amewasisitiza wataalamu wa taasisi hizo kutekeleza makubaliano hayo kwa vitendo wakijikita katika kutafuta suluhusho la changamoto zinazowakabili Wananchi.

“MoU hii iliyosainiwa hapa, mimi nafikiri ni jibu kubwa kabisa kwa tatizo letu sisi NBS, Teknolojia iweze kujibu matatizo ya Wananchi leo.” Amesema Mhe. Makinda.

Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amebainisha kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa NBS kushirikiana na taasisi hizo ili kupanua wigi wa kuzalisha Takwimu kwa kutumia methodolojia za kisasa ili kufikia na kufanikisha jukumu la kupima muenendo wa utekelezaji wa Dira 2050.

Amesema NBS inalenga kuimarisha uwezo wa watumishi wake kupitia mafunzo ya Teknolojia na programu mbalimbali huku ikishirikiana na UDSM pamoja na NM – AIST ili kuhakikisha mafunzo hayo yanaendana na mahitaji halisi ya Ofisi hiyo.

Naye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William-Andey Lazaro Anangisye amesema ushirikiano huo unaakisi utekelezaji wa Dira 2050 ambayo inasisitiza maendeleo ya rasilimali watu, sayansi, teknolojia, ubunifu na maarifa kwa ajili ya mageuzi ya kiuchumi.

Hivyo, amehimiza taasisi hizo kuweka programu madhubuti za utekelezaji wa makubaliano hayo, kubaini maeneo ya kipaumbele katika utafiti na kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti yanabadilishwa kuwa suluhisho la vitendo kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

Aidha, Makamu Mkuu wa Chuo cha NM – AIST, Prof. Maulilio John Kipanyula amesema maamuzi muhimu na makubwa nchini, hayawezi kujengwa kwa hisia au makisio, badala yake yanahitaji Takwimu rasmi zenye Ushahidi wa kisayansi.