NBS Accessibility Tools
NBS Accessibility Tools

Text Size

Language

Inflation Rate for August, 2026: 4.3% AASS 2023/2024 Women's Empowerment and Nutrition Module: WEN Tanzania Gender and Environment Survey: TGES 2025 Utafiti wa Kufuatilia Kaya (National Panel Survey, Wave 6: NPS 2026
The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

NBS, IHI Zaendesha Mafunzo Mifumo ya Taarifa za Kijiografia
Posted On: 18 September, 2026
NBS, IHI Zaendesha Mafunzo Mifumo ya Taarifa za Kijiografia

NBS, IHI Zaendesha Mafunzo Mifumo ya Taarifa za Kijiografia

Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya Ifakara - IHI zinaendesha mafunzo ya Mifumo ya Taarifa za Kijiografia katika Sekta ya Afya (Geospatial Modelling on Public Health) kupitia Mradi wa Malaria Atlas - MAP, kwa lengo la kuwajengea  uwezo watafiti na wataalamu kutumia mifumo hiyo katika kukusanya na kuchambua taarifa ili kuzalisha Takwimu rasmi.

Akifungua mafunzo hayo tarehe 15 Septemba 2026 katika Ukumbi wa Serengeti uliopo kwenye Jengo la Makao Makuu ya NBS jijini Dodoma, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema ushirikiano uliopo kati ya NBS na IHI kupitia mradi wa MAP una mchango mkubwa wa kuimarisha matumizi ya Takwimu rasmi katika kupanga, kutekeleza na kutathmini mipango na sera mbalimbali za maendeleo nchini.

Dkt. Msengwa amesema takwimu za kijiografia ni eneo muhimu na lenye utaalamu wa kipekee linalounganisha aina mbalimbali za taarifa, zikiwemo taarifa za kiuchumi, afya, idadi ya watu, kijamii na mazingira.

Kiongozi huyo amesema kwa kuhusisha taarifa za kitakwimu na mahali zinakotokea, takwimu za kijiografia zinawafanya wataalam kuelewa kwa undani maeneo yenye changamoto na namna changamoto hizo zinavyotofautiana kati ya jamii mbalimbali, pamoja na maeneo ambayo yanahitaji zaidi hatua za utekelezaji na rasilimali.

“Kwa asili yake, Takwimu za Kijiografia ni eneo linalohitaji ushirikiano wa taaluma mbalimbali. Linahitaji mchanganyiko wa ujuzi na utaalamu kutoka kwa wataalamu wa takwimu, wataalamu wa mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS), wanasayansi wa kompyuta, wataalamu wa magonjwa na afya ya jamii.” Amesema DKt. Msengwa na kuongeza;

“Utofauti huu wa utaalamu ni muhimu katika kuhakikisha kwamba taarifa zinaunganishwa, kuchambuliwa na kutafsiriwa kwa usahihi na hatimaye kubadilishwa kuwa ushahidi wenye maana na unaoweza kutumika katika kufanya maamuzi.”

Wakati huo huo, Dkt. Msengwa amesema ubunifu katika matumizi ya Takwimu unapaswa kwenda sambamba na ubora wa takwimu, uhuru wa kitaaluma, usiri wa taarifa, uwazi pamoja na mbinu thabiti na sahihi za kitakwimu.

Dkt. Msengwa amesisitiza kuwa anaiona warsha hiyo kuwa siyo tu kama mafunzo ya kitaalamu na kiufundi, bali ni fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya wataalamu wa takwimu rasmi na wataalamu wa afya ya umma, kuboresha matumizi ya taarifa za kijiografia na kujenga jumuiya ya wataalamu yenye uwezo wa kubadilisha taarifa na Takwimu kuwa ushahidi wa vitendo kwa ajili ya kuboresha matokeo ya afya ya jamii.

“Ofisi za Taifa za Takwimu inao msingi wa kisheria wa kitaifa na wa kimataifa wa uzalishaji na ulinzi wa taarifa, usambazaji na uratibu wa Takwimu rasmi nchini hivyo, kwa mtazamo huu, Takwimu Rasmi zina nafasi muhimu katika kuhakikisha kwamba taarifa zinazozalishwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa, zinapatikana kwa wakati, zinaaminika na zinaweza kutumika katika kupanga, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo.”

Naye, Mratibu wa Mradi wa MAP kutoka IHI, Dkt. Suza Rumisha amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanasaidia kuongeza uelewa na uwezo katika matumizi ya Takwimu rasmi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo wizara, taasisi, mashirika na wadau mbalimbali ili kufanya maamuzi yanayozingatia ushahidi wa kitakwimu.

Mafunzo hayo yanahusisha washiriki mbalimbali kutoka NBS, taasisi za Serikali, taasisi za elimu na utafiti, afya pamoja na wadau mbalimbali kutoka Tanzania, Kenya na Uganda ambapo yatafanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 15 hadi 18 Septemba 2026.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa makubaliano ya kushirikiana ya tarehe 17 julai 2026, baina ya taasisi hizo katika Matumizi ya Mifumo ya Taarifa za Kijiografia katika kukusanya na kuchambua Taarifa