NBS, OCGS Kuandaa Ripoti ya Kitaifa ya Hali ya Umaskini Usiotokana, Kipato
Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar – OCGS zinaandaa Ripoti ya Kitaifa ya Hali ya Umaskini Usitokana na Kipato – NMPI ya Mwaka 2016.
Ofisi hizo zimeandaa kikao cha wadau kwa ajili ya maandalizi ya uandaaji wa Ripoti hiyo kilichofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 13 hadi 14 Aprili 2026 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ngorongoro uliopo katika jengo la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Kassim Salum Ali amesema maandalizi ya ripoti hiyo ni hatua muhimu ya kuhakikisha Tanzania inakuwa na ushahidi wa kutosha wa kusaidia kufanya maamuzi sahihi ya kisera na kupanga mipango ya maendeleo yenye tija kwa Taifa kwa kuwa dhana ya umaskini usiotokana na kipato inatoa mtazamo mpana zaidi kwa kuangalia vipengele mbalimbali vinavyoathiri ustawi wa jamii, ikiwemo afya, elimu, mazingira, hali ya makazi, na upatikanaji wa huduma muhimu.
”Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaendelea kutumia takwimu rasmi na bora katika maendeleo ya taifa. Hivyo, tambueni kuwa uchambuzi wa taarifa za matokeo ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania – IHBS wa Mwaka 2025 unatupa mwanga mpana wa matokeo ya hali ya umasikini usio wa kipatao - MPI yatakayosaidia kubaini kwa usahihi makundi jamii na maeneo yaliyo katika hali ya umaskini, ili kuchukua hatua stahiki kwa wakati.” Amesema Kiongozi huyo.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Romward Dionis Rwamarumba, ametoa pongezi kwa NBS, OCGS, Tume ya Mipango Zanzibar pamoja na wadau wote kwa ushirikiano wao ambapo amesisitiza kuwa juhudi za kupunguza umaskini zimepewa kipaumbele cha juu katika mipango ya maendeleo nchini. Hivyo, aliwahimiza wadau wote kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni yenye tija, hususan kuhusu mbinu zilizotumika na viashiria vilivyojumuishwa, ili kuboresha ubora wa Ripoti hiyo.
Naye, mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto - UNICEF, Mlemba Abbas, alisisitiza kuwa lengo la kwanza la Malengo ya Maendeleo Endelevu - SDGs ni kutokomeza umaskini. Hivyo, amesema upimaji wa umaskini usiohusisha kipato unahusisha tathmini ya upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii, ikiwemo afya, maji safi na salama, elimu na lishe bora, hali ambayo huongeza uhalisia na ubora wa takwimu zinazokusanywa ambapo amepongeza ushirikishwaji wa wadau hao kuwa utawezesha kupata Ripoti shirikishi, jumuishi na yenye kuakisi uhalisia wa hali ya jamii.