The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
NBS, OCGS Waandaa Ripoti ya Utekelezaji wa Sensa
Posted On: 14 March, 2026
NBS, OCGS Waandaa Ripoti ya Utekelezaji wa Sensa

Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar - OCGS kwa ushirikiano na Sekratarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki - EAC zinaendesha mafunzo ya uandaaji wa Ripoti ya Utawala inayolenga kuelezea utekelezaji wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 katika awamu zote tatu za utekelezaji wa zoezi hilo. Mafunzo hayo yanayolenga kuimarisha utekelezaji wa Mwongozo wa EAC wa uandaaji wa Ripoti hiyo. Taarifa zinazojumuishwa kwenye ripoti hiyo zimejikita kwenye mafanikio, changamoto na uzoefu uliopatikana katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa lengo la kutumika kama rejea katika utelezaji wa Sensa ijayo na tafiti nyingine za kitakwimu ndani ya Mfumo wa Takwimu Nchini - NSS.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesisitiza kuwa sensa ni moja ya zoezi kubwa linaloratibiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambalo mafanikio yake yanatokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dkt. Msengwa amesema Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ilikuwa na mafanikio makubwa, ikiwemo matumizi ya teknolojia (vishikwambi) katika hatua zote za utekelezaji wake hasa wakati wa uandaaji wa ramani na kuhesabu watu.

Akirejea mafanikio ya Senza hiyo, Dkt. Msengwa alisisitiza kuwa, matumizi ya teknolojia yaliwezesha kukamilisha zoezi la Sensa kwa wakati na kuwezesha kutoa Matokeo ya Mwanzo takriban siku 45 baada ya kukamilika kwa zoezi la Kuhesabu Watu.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa ripoti ya utekelezaji wa sensa (Administrative Report) ni nyenzo muhimu inayochambua namna zoezi lilivyotekelezwa, mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza, ambazo zitasaidia kuboresha maandalizi ya sensa zijazo kama vile Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2032, Sensa za Kilimo na Sensa za Viwanda pamoja na tafiti nyingine, huku akiwahimiza wataalamu kutumia mafunzo hayo kukamilisha ripoti itakayokuwa rejea muhimu katika kuboresha mbinu na mifumo ya ukusanyaji wa takwimu nchini.

Aidha, Dkt. Msengwa ametoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kulipa kipaumbele zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa kuhakikisha rasilimali fedha, vifaa na watu vinapatikana kwa wakati, hali iliyosaidia wataalamu wa takwimu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mwakilishi kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ndugu Mose Job amesema, hatua hiyo inalenga kuimarisha ubora wa nyaraka za sensa pamoja na kuoanisha utekelezaji wa shughuli za sensa katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.

Job amesema Mwongozo wa pamoja wa EAC wa uandaaji wa ripoti za kiutawala za sensa unasaidia kuoanisha mbinu za utekelezaji wa sensa ikiwemo uandaaji wa ramani za sensa, mbinu za ukusanyaji wa takwimu sambamba na kuoanisha nyenzo zinazotumika na nchi wanachama  ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.                                                                                                                                                                                                 

Naye, Meneja wa Sensa ya Watu na Takwimu za Matukio Muhimu ya Binadamu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ndugu Seif Kuchengo, amesema mafunzo hayo yanahusisha wataalamu kutoka NBS, OCGS pamoja na wadau kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki, yakilenga kuhakikisha ripoti ya utekelezaji wa zoezi la sensa inaandaliwa kwa kuzingatia miongozo na vigezo vya kikanda na kimataifa ambapo hadi sasa Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kutekeleza mwongozo huo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.