NBS, OCGS Zaanza Majaribio Utafiti NPS 2026
Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar - OCGS zimeanza zoezi la majaribio kwa Wadadisi na Wasimamizi wa Utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya (National Panel Survey - NPS) 2026 katika Kijiji cha Nzihi, Kata ya Nzihi, Wilaya ya Iringa mkoani Iringa ikiwa ni sehemu ya kukamilisha mafunzo ya nadharia kabla ya kuanza utafiti rasmi nchini.
Akizungumza uwandani wakati wa zoezi hilo leo tarehe 04 Agosti 2026, Meneja wa Idara ya Tafiti, Viwango na Ubunifu, Mariam Kitembe amesema baada ya kukamilisha mafunzo ya darasani, wadadisi na wasimamizi wanaendelea na mafunzo kwa vitendo kupitia zoezi la majaribio yatakayofanyika kwa siku tatu.
“Kwa sasa tupo katika mafunzo kwa vitendo na wadadisi pamoja na wasimamizi hatua ambayo ni muhimu katika Utafiti huu...tunapata nafasi ya kutathmini ufanisi wa mafunzo yaliyotolewa darasani na kuwaandaa wadadisi pamoja na wasimamizi kabla ya kuanza rasmi zoezi la ukusanyaji wa Takwimu. Amesema Kitembe na kuongeza;
“Baada ya kukamilisha mafunzo haya, watatawanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kukusanya taarifa za Utafiti huo kwa Kaya zitakazochaguliwa...natoa wito kwa Wananchi katika Kaya hizo kutoa ushirikiano kwa Wadadisi kwani taariofa sahihi huzalisha Takwimu rasmi ambazo huisaidia Serikali pamoja na wadau kupanga mipango yenye tija kwa Wananchi.”
Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Nzihi, Joseph Kalinga amesema kuwa kijiji hicho kimewapokea Wataalam hao na wao kama viongozi wapo tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha majaribio ya Utafiti huo ambapo vitongoji vinne vitatembelewa kwa siku mbili.