NBS, OCGS Zaanza Uandishi wa Ripoti Mbili Arusha
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), imeanza kikao kazi cha uandishi wa Ripoti ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi nchini pamoja na Ripoti ya Umaskini Usiotokana na Kipato nchini za mwaka 2025, zoezi ambalo linafanyika kwenye Ukumbi wa Mafao Village, jijini Arusha.
Kikao hicho kinahusisha wataalamu kutoka wizara, taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na wadau wa maendeleo, na kinafanyika kwa muda wa siku 10 kuanzia tarehe 17 hadi 26 Mei 2026.
Uandishi wa ripoti hizo umeanza mara baada ya kukamilika kwa ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi uliofanyika nchini kote.
Matokeo ya tafiti hizo yanatarajiwa kusaidia kupima na kutathmini hali ya umaskini nchini, kufanya maamuzi ya kisera yanayotegemea ushahidi wa kitakwimu pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa ikiwemo Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 1), Ajenda 2063 na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.