NBS Accessibility Tools
NBS Accessibility Tools

Text Size

Language

AASS 2023/2024 Women's Empowerment and Nutrition Module: WEN Tanzania Gender and Environment Survey: TGES 2025 Utafiti wa Kufuatilia Kaya (National Panel Survey, Wave 6: NPS 2026 Tanzania Inflation Rate April 2026: 4.0 %
The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

NBS, TASAC Zasaini Makubaliano Kufanya Sensa Vyombo vya Usafiri Majini
Posted On: 04 June, 2026
NBS, TASAC Zasaini Makubaliano Kufanya Sensa Vyombo vya Usafiri Majini

Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS kwa kushirikiana na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania - TASAC, zimesaini Makubaliano ya Ushirikiano - MoU kufanya Sensa ya Vyombo vya Usafiri wa Majini na Wajenzi wa Meli Tanzania Bara Mwaka 2026/2027 ili kupata Takwimu rasmi zitakazosaidia kuboresha usimamizi na maendeleo ya sekta hiyo.

Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha upatikanaji wa takwimu rasmi, za kuaminika na za kisasa zitakazosaidia kupanga, kusimamia na kuendeleza sekta ya usafiri majini nchini. Sensa hiyo itakuwa ya pili kufanyika nchini baada ya sensa ya kwanza iliyofanyika Mwaka 2021 kwa ushirikiano wa NBS na TASAC.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano huo, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ngorongoro uliopo Jengo la Makao Makuu ya NBS jijini Dodoma leo tarehe 03 Juni 2026, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema hiyo ni hatua muhimu itakayowezesha uratibu wa mfumo wa Takwimu rasmi nchini na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa ajili ya kuiwezesha Serikali na wadau kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa Wananchi.

Dkt. Amina Msengwa, amesema sensa hiyo itasaidia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya Serikali, ikiwemo kuimarisha mfumo wa usafirishaji fungamanishi nchini ambapo Takwimu zinazopatikana kupitia sensa hiyo zitakuwa ni nyenzo muhimu katika kufanya maamuzi sahihi ya kisera, kupanga uwekezaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, ameishukuru TASAC kwa kuendelea kushirikiana na NBS katika utekelezaji wa zoezi hilo muhimu, akieleza kuwa ushirikiano huo unaimarisha juhudi za Serikali za kuhakikisha upatikanaji wa takwimu bora, za kuaminika na zinazokidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa.

“Takwimu hizo zitasaidia kubainisha idadi na aina za vyombo vinavyofanya kazi nchini, kufuatilia utekelezaji wa kanuni za usalama majini na kuweka msingi imara wa usimamizi bora wa sekta ya usafiri wa majini.” Amesema Dkt. Msengwa na kuongeza;

“Tukifahamu hali halisi ya sekta hii kwa ukamilifu, tutakuwa na msingi imara wa kupanga na kutekeleza uwekezaji unaolenga kuimarisha usafirishaji wa wananchi na bidhaa nchini,”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, amesema sensa hiyo ni hatua muhimu katika kuhuisha kanzidata ya kitaifa ya vyombo vya usafiri majini na kupata taarifa sahihi kuhusu vyombo vinavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.

Salum ameongeza kuwa matokeo ya sensa yatasaidia kuboresha usimamizi wa usalama majini, kuimarisha utekelezaji wa sheria na kanuni, pamoja na kusaidia maamuzi ya kisera, kiudhibiti na kiuwekezaji katika sekta hiyo.

Takwimu zitakazopatikana zitatumika kuimarisha usalama wa vyombo na abiria, kuboresha upangaji wa miundombinu ya usafiri majini, kuchochea uwekezaji katika uchumi wa buluu na kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.