NBS, UNDP Kuimarisha Ushirikiano katika kufanya Utafiti wa Watu Wenye Ulemavu
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS, Dkt. Amina Msengwa amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe maalum kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo - UNDP kwa lengo la kufanya tathmini ya kina kuhusu uchambuzi wa sera, mikakati na mipango ya huduma, malezi na matunzo kwa wasaidizi wa kazi wanaolipwa na wasiolipwa (paid and unpaid care support).
Akizungumza na ujumbe huo ofisini kwake jijini Dodoma kiongozi huyo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo, hususan katika kuboresha upatikanaji wa takwimu za watu wenye ulemavu nchini.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kazi za Mifumo Isiyo na Malipo, Ulemavu na Jinsia kutoka UNDP, Ghati Horombe, amesema Shirika hilo kwa sasa linaweka mkazo katika masuala ya jinsia, ulemavu, uongozi na sera, kupunguza umasikini pamoja na uhifadhi wa mazingira, miongoni mwa maeneo mengine yanayohusiana na maendeleo jumuishi.
Naye, Mtakwimu Mwandamizi na Mratibu wa Takwimu za Ulemavu kutoka - NBS, Mdoka Omary, amebainisha kuwa ushirikiano huo ni fursa muhimu kuelekea utekelezaji wa Utafiti wa Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2026/2027, ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano ambapo ameongeza kuwa ujio wa UNDP utarahisisha upatikanaji wa utaalamu na rasilimali zitakazochangia kufanikisha utafiti.