The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
NBS Yaanza Rasmi Uimarishaji Mfumo wa M&E
Posted On: 18 March, 2026
NBS Yaanza Rasmi Uimarishaji Mfumo wa M&E

Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS imeanza rasmi uimarishaji wa Mfumo wa Ufuatilaji na Tathmini – M&E kwa kikao kazi cha kuandaa nyaraka ya utayari wa Mfumo huo pamoja na mwongozo wa uendeshaji wake, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa shughuli za taasisi.

Akifungua kikao hicho, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa NBS, Petronila Shirima amesisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo madhubuti wa M&E katika kufanikisha malengo ya taasisi.

“Mfumo imara wa M&E unatuwezesha kupata taarifa sahihi kwa wakati, kupima mafanikio shughuli zote na kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi.” Amesema Shirima.

Pia, kwa NBS uimarishaji wa mfumo huo ni wa kimkakati kutokana na jukumu lake la kuzalisha takwimu rasmi na kuratibu Mfumo wa Taifa wa Takwimu.

Aidha, kikao hicho kimehusisha wataalamu wa Ufuatilaji na tathmini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Msajili wa Hazina na wataalamu kutoka ofisi ya Taifa ya Takwimu ili kufanya tathmini ya kina ya utayari wa taasisi na kuandaa mwongozo utakaoboresha ukusanyaji wa taarifa, ufuatiliaji wa viashiria na utoaji wa ripoti.

Kikao kazi hicho kinatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu.