The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
NBS Yampokea Mwenyekiti Mpya wa Bodi
Posted On: 21 February, 2026
NBS Yampokea Mwenyekiti Mpya wa Bodi

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa tarehe 20 Februari 2026 ameingoza Menejimenti na Watumishi wa Ofisi hiyo kumpokea rasmi Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mhe. Anne Semamba Makinda ambaye ameteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Makinda amewasili Makao Makuu ya NBS katika Jengo la Takwimu lililopo Barabara ya Lusinde Mtaa wa Tambukareli jijini Dodoma, majira ya saa 04:00 asubuhi ambapo mara baada ya kupokelewa, kusaini Kitabu cha Wageni alipata nafasi ya kuzungumza na watumishi wa Ofisi hiyo waliopo Makao Makuu kwenye Ukumbi wa Ngorongoro.

Akizungumza awali Dkt. Msengwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mhe. Makinda kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya NBS ili Ofisi hiyo iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Mhe. Makinda kwa niaba ya Menejimenti na Watumisho wote wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu tunakupongeza sana kwa uteuzi wako...aidha, kipekee nimshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa na imani kubwa na wewe katika masuala ya uongozi na kukuteua kwa nafasi hii.” Amesema Dkt. Msengwa na kuongeza;

“Kadhalika, tunakushukuru sana, wewe hapa NBS siyo mgeni, tumekuwa na wewe ukiwa Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na kipekee ulituonesha ushirikiano mkubwa katika kipindi chote cha uongozi wako, uliweza kuuza, kutoa takwimu na kuzisemea umuhimu wake katika kutekeleza mipango ya Serikali, wadau na jamii kwa ujumla.”

Dkt. Msengwa amemuarifu Mwenyekiti huyo kuwa Menejimenti kwa sasa ipo kwenye maandalizi ya kuandaa Mpango Makakati - SP mpya (2026/2027 hadi 2030/2031), kutokana na Mpango Mkakati wa awali (2021/2022 hadi 2025/2026) kufikia ukingoni Mwezi Juni 2026.

Kadhalika, amesema ili kupata data na takwsimu jumuishi, NBS inaendelea kuboresha mifumo ya upatikanaji wa takwimu kwa kushirikiana na taasisi pamoja na wizara ili mifumo hiyo iweze kusomana kwani mpaka sasa ni taasisi na wizara 11 tayari mifumo yake imefanikiwa kuungwanishwa na Mfumo wa Data wa NBS ambapo malengo ni kufikia taasisi na wizara 20 ifikapo Juni 2026.

Dkt. Msengwa ameweka wazi kuwa kipaumbele kingine ni namna bora ya kutekeleza majukumu ya taasisi kwa ufanisi zaidi kwa kuboresha mifumo ya kiteknolojia na kujengeana uwezo wa kutumia mifumo hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi Anne Semamba Makinda amemshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya NBS ambapo ameahidi kuilinda imani hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii kufikia malengo mahususi huku akiwashukuru Watumishi hao kwa mapokezi na ameahidi kuwapa ushirikiano kama alivyoutoa wakati akiwa Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Pia, Mhe. Makinda amesema yeye pamoja na Wajumbe wa Bodi waliochaguliwa, watahakikisha  majukumu ya NBS yanajulikana ipasavyo kwa umma na watunga sera kwani takwimu zinazozalishwa na Ofisi hiyo ndizo zinazotumika na Serikali pamoja na Wadau wa Maendeleo katika kupanga na kutekeleza mipango na mikakati ya maendeleo.