The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
NBS Yampongeza Dkt. Chuwa
Posted On: 05 February, 2026
NBS Yampongeza Dkt. Chuwa

Menejimenti na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS inampongeza Dkt. Albina Andrew Chuwa, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mstaafu kwa kuteuliwa na Kamati Tendaji ya Taasisi ya Kimataifa ya Takwimu – ISI, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Maadili (Advisory Board for Ethics – ABE) ya Taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka minne.

Kamati hiyo imetangaza rasmi uteuzi wa Dkt. Albina Andrew Chuwa tarehe 21 Januari 2026 akichukua nafasi ya Profesa Walter Josef Radermacher wa Ujerumani, ambaye ameiongoza Bodi hiyo kwa umahiri mkubwa kwa kipindi cha miaka minne (2022 hadi 2025).

Dkt. Chuwa anakuwa Mwafrika wa kwanza kuiongoza Bodi hiyo tangu Taasisi hiyo ianzishwe mwaka 1885 na kwamba mabadiliko hayo yanaashiria hatua muhimu kwa ISI katika kuendelea kusimamia na kuendeleza Kanuni za Maadili ya Kitaaluma katika jamii ya takwimu duniani.

NBS inatambua kuwa heshima hiyo si tu kwa Dkt. Chuwa, bali ni heshima ya Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa Bodi ya Ushauri ya Maadili ina jukumu muhimu la kimataifa la kusimamia utekelezaji wa maadili katika takwimu, kutoa ushauri kuhusu changamoto tata za matumizi ya takwimu na data, na kuhakikisha uadilifu wa takwimu unabaki kuwa msingi wa maamuzi ya kimataifa.

Uteuzi wa Dkt. Chuwa unaonesha uzoefu wake mkubwa katika usimamizi wa data na dhamira yake ya kuendeleza ajenda ya “Kutomuacha Mtu Nyuma” kupitia matumizi sahihi na yenye maadili ya data.

“Nimeheshimiwa sana kuaminiwa na Kamati Tendaji ya ISI kupewa jukumu hili…katika zama hizi za ‘Big Data’ na maendeleo ya haraka ya Akili Unde - AI, matumizi ya takwimu kwa kuzingatia maadili ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote ili kudumisha imani ya umma. Natarajia kuendeleza msingi uliowekwa na Profesa Radermacher na kushirikiana na wenzangu duniani kote kulinda viwango vya juu vya taaluma yetu.” Amesema Dkt. Chuwa.

Chini ya uongozi wake, Bodi ya Ushauri inatarajiwa kuangazia zaidi changamoto za faragha ya taarifa, matumizi ya kimaadili ya taarifa za kiutawala, na kuziba pengo kati ya Ofisi za Taifa za Takwimu na mifumo ya kimataifa ya maadili.

Aidha, kabla ya uteuzi huo, Dkt. Chuwa amewahi kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Taasisi ya Kimataifa ya Takwimu – ISI kwa kipindi cha miaka mitano (2019 hadi 2023) hali ambayo inadhihirisha uzoefu wake katika Taasisi hiyo yenye makao yake makuu The Hegue, Uholanzi.