The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
NBS Yawajengea Uwezo Mameneja Takwimu Mikoa
Posted On: 16 April, 2026
NBS Yawajengea Uwezo Mameneja Takwimu Mikoa

Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS inaendesha mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wa kitaalamu katika ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa takwimu rasmi na zenye ubora, kwa Mameneja Takwimu mikoa wote Tanzania Bara kwa lengo la kutoa mafunzo ya nyenzo zitakazotumika kukusanyia taarifa kwa ajili ya kuandaa Wasifu wa Mikoa Tanzania Bara yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Midland Dodoma kuanzia tarehe 13 hadi 20 Aprili 2026.

Akifungua mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa NBS, Mhe. Anne Semamba Makinda, amewataka Mameneja hao kuwa mabalozi wazuri wa taasisi hiyo huku wakizingatia uadilifu na misingi ya kazi na taaluma hiyo.

Aidha, pamoja na ufunguzi wa mafunzo hayo Mhe. Makinda aliwasilisha mada kuhusu masuala ya Uongozi ambapo amesisitiza umuhimu wa kuwa viongozi bora wanaosikiliza, wanaofuata maadili ili kuleta tija kwa Taasisi hiyo muhimu nchini.

Kwa upande wake, Kaimu Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Ruth Minja, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uzalishaji wa takwimu katika ngazi za mikoa na halmashauri, huku akibainisha kuwa Wasifu wa Mikoa utaonyesha fursa zilizopo, changamoto pamoja na hali halisi ya maendeleo katika maeneo husika huku akiwataka kuwa walimu na mabalozi wa takwimu katika maeneo yao ili kuhakikisha ubora na matumizi sahihi ya takwimu rasmi, unaimarika kuanzia ngazi za Halmashauri.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Uratibu, Tafiti na Shughuli za Kitakwimu wa NBS, James Mbongo, amesema mafunzo hayo pia yamelenga kutoa nafasi kwa wataalam hao kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora kutoka mikoa mbalimbali, jambo ambalo anaamini litasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuleta chachu mpya katika uzalishaji wa takwimu rasmi na bora, zitakazosaidia kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa ufanisi zaidi nchini.