Rc Senyamule Awasisitiza Wanawake Kuongeza Uthubutu
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewasisitiza wanawake kutumia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kutathmini hatua mbalimbali zilizofikiwa katika kuleta usawa wa kijinsia na kuongeza bidii katika kupigania haki na fursa za kiuchumi kwa Wanawake mkoani humo na taifa kwa ujumla.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kwa Mkoa wa Dodoma yamefanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mbande wilayani Kongwa leo tarehe 8 Machi 2026 ambapo Kiongozi huyo ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.
Kiongozi huyo amesema, maadhimisho hayo ambayo hufanyika duniani kote kila mwaka ifikapo tarehe 08 Machi, inapaswa kuwa chachu ya kuhamasisha jamii kuendelea kuunga mkono wanawake wanaoonyesha njia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Mafanikio ya mwanamke hayaji kirahisi, kuna kupambana na uvumilivu mkubwa. Hata hivyo, tusikate tamaa kwani kwa mshikamano na uwezo tulionao tunaweza kufika mbali; tusimame imara tutavuka.” Amesema Senyamule.
Akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, Meneja wa Utafiti wa Viwango na Ubora, Mariam Kitembe ameeleza kuwa takwimu zinazozalishwa na taasisi hiyo ni nyenzo muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya wanawake.
Pia, Kitembe ameongeza kuwa takwimu hizo huisaidia Serikali na wadau mbalimbali kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa, ikiwemo huduma za vituo vya afya ili kupunguza vifo vya mama na mtoto, pamoja na kuimarisha usawa wa kijinsia kuanzia ngazi ya kaya hadi ngazi za kitaifa kupitia sera na mipango mbalimbali ya maendeleo.
Awali, RC Senyamule ametembelea Banda la Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS lilikuwa uwanjani hapo ambapo amejionea takwimu mbalimbali zinazohusu wanawake na jinsia pamoja na namna zinavyotumika katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.
Katika banda la NBS, Mhe. Senyamule amepata maelezo kuhusu umuhimu wa takwimu sahihi katika kuimarisha usawa wa kijinsia, kufanya maamuzi sahihi ya maendeleo na kuboresha ustawi wa wanawake katika jamii.