SG Dkt. Msengwa Afungua Kikao Uchambuzi IHBS 2025 Ikiwa ni Maandalizi ya Ripoti ya EAC - MPI
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, Dkt. Amina Msengwa amefungua kikao kazi cha siku tano cha uchambuzi wa taarifa za Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania (Integrated Household Budget Survey - IHBS) za Mwaka 2025 kwa ajili ya kuandaa ripoti ya Umaskini Usiotokana na Kipato (Multidimensional Poverty Index - MPI) kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kinachofanyika Hoteli ya Rafiki jijini Dodoma tarehe 14 Julai 2026.
Dkt. Msengwa ameishukuru Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuendelea kuongoza juhudi za kuoanisha takwimu rasmi katika ukanda huo hususan dhamira ya Tanzania ya kuimarisha utungaji wa sera unaotegemea ushahidi kupitia takwimu za kikanda zilizoidhinishwa kwa viwango vinavyofanana, pamoja na Benki ya Dunia kwani ushirikiano huo umeiwezesha Tanzania kuzalisha Takwimu za pande zote mbili (Tanzania Bara na Zanzibar).
Kiongozi huyo ameeleza kuwa NBS imepiga hatua kubwa tangu kukamilika kwa ukusanyaji wa taarifa za IHBS mwezi Disemba 2025, ikiwemo uzalishaji na uchapishaji wa makadirio ya kitaifa ya umaskini wa kipato, pamoja na takwimu za kikanda, mijini na vijijini na kuwa Tanzania inaendeea na uandaaji wa ripoti ya NMPI, ambayo kwa sasa ipo katika hatua ya uhakiki kabla hazijawasilishwa kwa wadau.
Dkt. Msengwa amefafanua Takwimu hizo zitatumka kutathmini hali ya upatikanaji wa huduma na fursa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, makazi na huduma nyingine za msingi na hivyo kuwapatia watunga sera uelewa mpana zaidi wa umaskini ili kuwezesha utekelezaji wa afua zinazolenga kuboresha ustawi wa Wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Lengo la Kwanza la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), la kutokomeza umaskini wa aina zote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Aime Uwase, amesema kuwa kikao hicho ni sehemu ya mchakato wa kila mwaka wa kuhuisha EAC MPI ili kuhakikisha takwimu za umaskini zinaendelea kuwa za wakati uliopo na zinazoweza kulinganishwa miongoni mwa Nchi Wanachama wa EAC.
Amesema washiriki wanatarajiwa kushirikiana kukokotoa MPI iliyohuishwa, kutafsiri matokeo na kuandaa mchango wa Tanzania katika Ripoti ya EAC MPI ya mwaka 2025 ambapo amewahimiza washiriki kubadilishana uzoefu na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuandaa wasifu wa umaskini ulio imara na wenye ubora.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Matukio Muhimu ya Binadamu, Cosmas Stephano, amesema MPI iliyohuishwa itawapatia watunga sera uelewa wa kina zaidi kuhusu vipengele mbalimbali vya umaskini, pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa maendeleo katika utekelezaji wa Lengo la Kwanza la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ambalo ni kutokomeza umasikini wa aina zote.
Stephano amesema kuwa zoezi hilo pia litaongeza matumizi ya Takwimu za Utafiti wa IHBS katika kuandaa sera za kikanda na mipango ya maendeleo kupitia wasifu wa umaskini ulio imara na unaoweza kulinganishwa.
Kikao kazi hicho kinajumuisha wataalamu kutoka NBS na taasisi nyingine za Serikali na Wataalamu kutoka Sekretarieti ya EAC.