NBS Accessibility Tools
NBS Accessibility Tools

Text Size

Language

AASS 2023/2024 Women's Empowerment and Nutrition Module: WEN Tanzania Gender and Environment Survey: TGES 2025 Utafiti wa Kufuatilia Kaya (National Panel Survey, Wave 6: NPS 2026 Tanzania Inflation Rate April 2026: 4.0 %
The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

SG Dkt. Msengwa: Fahamuni Sura za Maeneo Mnayofanyia Kazi
Posted On: 13 May, 2026
SG Dkt. Msengwa: Fahamuni Sura za Maeneo Mnayofanyia Kazi

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amewahimiza Wataalam wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kufahamu vema sura na idadi ya watu katika maeneo yao hususan katika uandaaji wa Wasifu wa Kijamii na Kiuchumi wa mikoa na Halmashauri hizo, ili kupata Takwimu zenye ushahidi wa kina na tija kwa matumizi ya mipango ya Serikali na wadau wa maendeleo nchini.

Dkt. Msengwa ameyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya uandaaji wa Wasifu wa Kijamii na Kiuchumi wa Mikoa na Halmashauri kwa njia ya mtandao akiwa kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma hivi karibuni.

“Kwa nafasi hii maana yake tutakuwa na Wasifu ambao utakuwa na Takwimu za kiuchumi lakini pia za kijamii, na kama mnavyofahamu za kijamii kuna ambazo mtazalisha huko lakini nyingi pia zipo kwenye ripoti mbalimbali, kwa hiyo fursa hii ni fursa muhimu ya kuhakikisha kwamba tunafahamu maeneo tunayofanyia kazi yana sura gani, kwa kuanzia kuangalia population (idadi ya watu) yenyewe na mambo mengine yote ya kijamii.” Amesema Dkt. Msengwa na kuongeza;

“Pia, tunaweza kukokotoa kuona structure (muundo) ya uchumi wa eneo husika...kwa bahati kabla sijaja kufungua mafunzo haya kitaifa ambayo nayafanyia hapa Ofisi za Mkoa Dodoma, nimekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Mkoa huu, Dkt. Khatibu Malimi Kazungu naye ametuambia kwa Dodoma tu hapa structure (muundo) yake ya uchumi anaiona katika maeneo matano ya kilimo, viwanda, madini, logistics (usafirishaji) na utalii...ukiangalia mnyambuliko huo je, tunaiona hiyo structure kwenye uchumi ambao sisi tunaupima kitakwimu?” 

Kiongozi huyo ametoa rai kwa washiriki wote nchini kutambua kuwa wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha kila Mkoa na kila Halmashauri zinapata Wasifu katika maeneo yao ili kuwezesha utekelezaji wa mipango ya taifa hususan Dira 2050.

Ikumbukwe kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa Waraka uliotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukizitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuandaa Wasifu huo, ili kuzalisha Takwimu rasmi zitakazoiwezesha Serikali pamoja na wadau kupanga vema mipango ya maendeleo kutokana na mahitaji yaliyopo.