The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Wadadisi 114 Wapatiwa Mafunzo ya Utafiti wa FINSCOPE MSME
Posted On: 08 March, 2026
Wadadisi 114 Wapatiwa Mafunzo ya Utafiti wa FINSCOPE MSME

Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar - OSGS kwa kushirikiana na wadau wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania - FSDT wametoa mafunzo ya siku 13 kwa Wadadisi ili kuwajengea uwezo wa kukusanya taarifa za Utafiti wa Huduma za Kifedha kwa wafanyabiashara wadogo sana, wadogo na wa kati.

Mafunzo hayo ambayo yanahusisha Wadadisi 114 watakao fanya kazi ya ukusanyaji wa taarifa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar, yanafanyika kwenye Ukumbi wa Mount Uluguru Morogoro mjini kuanzia tarehe 25 Februari hadi tarehe 09 Machi 2026.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mtakwimu ambaye pia ni Afisa Dawati wa Utafiti huo, Herman Kashililika amesema kuwa Utafiti huo ni wapili kufanyika nchini ambapo kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 2010.

Kashililika amesema utafiti huo utasaidia kuboresha taarifa za mwaka 2010 na kutoa tathmini ya mabadiliko ya sekta ya fedha kwa biashara ndogo yaliyo ambatana na ukuaji mkubwa wa teknolojia, kukadiria wigo wa biashara ndogo, kutambua na kueleza sehemu mbalimbali za soko, fedha zenye mahitaji maalumu, kutambua vichocheo na vikwazo vya upatikanaji wa huduma za kifedha kwa biashara ndogo na kueleza viwango na mazingira ya upatikanaji wa bidhaa na huduma za fedha.

Aidha, Kashilika amefafanua kuwa Utafiti huo utaongeza taarifa mpya za masuala ya kifedha ya MSME nchini Tanzania ambapo utatumia sampuli wakilishi ya kitaifa ambapo takriban maeneo 815 ya kuhesabia watu katika mikoa 31 ya Tanzania (Mikoa 26 kutoka Tanzania Bara maeneo 695 na Mikoa 5 kutoka Zanzibar maeneo 120 yatahusika) Wadadisi watatembelea biashara 815 nchi nzima.

Kashililika amesema lengo kuu la utafiti huo ni kupima na kuelezea viwango vya upatikanaji na matumizi ya huduma za kifedha kwa biashara na viwango mbalimbali vya kipato na viashiria vingine vya kitakwimu, na kutoa taarifa kwa wadau wakuu kama watunga sera, wasimamizi (Regulator) na watoa huduma za kifedha.