Wadadisi Utafiti wa FinScope MSMEs Wafanya Mazoezi kwa Vitendo Uwandani
Wadadisi watakaoshiriki zoezi la kukusanya taarifa za Utafiti wa Huduma za Fedha kwa Wafanyabiashara Wadogo, Wadogo Sana na wa Kati - FinScope MSMEs wamefanya mazoezi kwa vitendo uwandani kwa siku mbili (tarehe 06 na 07 machi 2026) katika Mtaa wa Mazimbu Darajani, Kata ya Mazimbu, Manispaa ya Morogoro ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Utafiti huo wa Mwaka 2025/2026.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mtakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu -NBS, Neema Martin Madembwe amesema zoezi hilo la majaribio linafanyika baada ya Wadadisi kupatiwa mafunzo maalum kabla ya kuanza rasmi ukusanyaji wa taarifa.
“Leo tupo kwa ajili ya mazoezi ya uwandani baada ya kupata mafunzo kwa wadadisi. Tunafanya mazoezi haya ili kujiandaa vizuri kabla ya kuanza rasmi zoezi la ukusanyaji taarifa.” Amesema Madembwe.
Madembwe ameongeza kuwa lengo la mazoezi hayo ni kuwajengea uzoefu Wadadisi katika ukusanyaji wa taarifa ili kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kutoka kwa Wafanyabiashara watakaoshiriki kwenye utafiti huo.
Aidha, ametoa rai kwa Wadadisi kuhakikisha wanapata taarifa zenye ubora na kuhakikisha kwamba usiri wa taarifa zinazokusanywa unazingatiwa kwa hari ya juu hasa wanapokuwa wanafanya mahojiano na kaya au biashara ambazo zitafikiwa.
Akizungumza moja ya Wadadisi wa Utafiti huo, Elias Shengoma, amesema zoezi la majaribio ya uwandani limewasaidia kuona uhalisia kwa vitendo baadhi ya changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa zoezi la ukusanyaji wa taarifa litakapo anza rasmi.
“Zoezi hili linatupa picha halisi ya mazingira ya kazi na changamoto zinazoweza kujitokeza hivyo, linatusaidia kujiandaa vizuri kabla ya kuanza zoezi rasmi la utafiti.” Amesema Shengoma.
Utafiti wa FinScope MSMEs unalenga kukusanya taarifa sahihi kuhusu upatikanaji na matumizi ya huduma za fedha kwa wafanyabiashara wadogo sana, wadogo na wa kati nchini, ili kusaidia wadau mbalimbali kuboresha sera na mipango ya maendeleo ya sekta hiyo.