Wataalam Tabora Wanolewa Kuandaa Wasifu wa Mkoa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora imeendesha mafunzo maalum ya uandaaji wa Wasifu wa Kijamii na Kiuchumi wa Mkoa (Regional Socio-Economic Profile), yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa TACTIC, Manispaa ya Tabora.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo yanayohusisha washiriki kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa wa Tabora pamoja na wataalam kutoka idara na taasisi za umma ndani ya mkoa huo, Mchumi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Lucas Chacha ameeleza kuwa lengo kuu ni kuwajengea uwezo wataalam hao ili waweze kuandaa kwa weledi Wasifu wa Kijamii na Kiuchumi wa Mkoa wa Tabora kwa kuzingatia viwango vya kitaalam vya ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa Takwimu.
Chacha amesema Wasifu huo unatarajiwa kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi zitakazowezesha kufanya tathmini na ulinganisho wa maendeleo ya Mkoa wa Tabora katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi, pamoja na kusaidia mipango ya maendeleo na utoaji wa maamuzi yenye tija kwa Wananchi hususan katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Mafunzo hayo yanafanyika katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuimarisha matumizi ya Takwimu katika upangaji na utekelezaji wa shughuli za maendeleo nchini.
CHANZO: Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora