Mhe. Sangu Aipongeza NBS Uzalishaji Takwimu Rasmi Nchini
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (Mb), ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS kwa kazi kubwa ya kukusanya, kuchakatana kusambaza Takwimu rasmi zinazotumiwa na Serikali pamoja na wadau katika kupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ya Taifa.
Mhe. Sangu ametoa pongezi hizo leo tarehe 24 Septemba 2026 alipotembelea Banda la NBS kwenye Maonyesho ya Tisa ya Kimataifa ya Madini yaliyoanza yanayofanyika kwenye Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili mkoani Geita, akieleza kuwa Takwimu rasmi ni msingi muhimu katika kufanya maamuzi na kupanga maendeleo ya nchi.
Amesema NBS inafanya kazi nzuri katika kuhakikisha Serikali na wadau mbalimbali wanapata Takwimu zinazohitajika kwa ajili ya mipango na utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika maeneo mbalimbali.
“NBS wanafanya kazi nzuri, bila wao hakuna mipango inaenda.” Amesema Mhe. Sangu huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ukusanyaji, uchambuzi na utunzaji wa Takwimu rasmi nchini.
Amesema Takwimu zinazozalishwa na taasisi hiyo zina mchango mkubwa katika kuisaidia Serikali kutambua mahitaji ya wananchi, kuweka vipaumbele na kupanga mikakati ya maendeleo yenye kuzingatia hali halisi ya Taifa.
Mhe. Sangu ameitaka NBS kuendelea kuisadia Serikali kufikia malengo yake kwa kuhakikisha Takwimu zinapatikana kwa wakati na zinatumika ipasavyo katika utekelezaji wa mipango Taifa.
Aidha, amesema kazi hiyo ni muhimu katika safari ya utekelezaji wa Dira 2050, ambayo inalenga kuweka msingi wa maendeleo endelevu na kuboresha maisha ya Watanzania.
Ameipongeza NBS kwa ushiriki wake katika Maonyesho ya Tisa ya Kimataifa ya Madini, akisema maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi na wadau kupata uelewa kuhusu kazi zinazofanywa na taasisi hiyo pamoja na umuhimu wa takwimu katika sekta mbalimbali za Uchumi.