Tafiti Nne za NBS Zawasili Jilawi Ziwafikie Wananchi
Matukio katika picha ni Meneja Takwimu za Viwanda na Ujenzi, Veronica Mwangoka na Meneja wa Takwimu za Mazingira na Makazi, Stephano Cosmas wote wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mahojiano katika Kipindi cha Jilawi cha TBC Radio Jamii Dodoma (93.7) tarehe 16 Machi 2026.
Ofisi hiyo inaendelea na tafiti nne muhimu za kiuchumi zenye lengo la kuboresha ukusanyaji wa taarifa ili kuzalisha Takwimu zitakazosaidia Serikali na Wadau kupanga mipango mbalimbali kwa maendeleo ya uchumi nchini.
Wataalam hao wamesema miongoni mwa tafiti hizo ni Utafiti wa kina wa shughuli za biashara, unaolenga kuchambua shughuli zote zinazozalisha kipato kupitia utoaji wa huduma na biashara mbalimbali.
Aidha, mahojiano hayo yamefanyika ikiwa ni siku chache (7) tangu Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, atangaze kupitia Mkutano wake na Vyombo vya Habari kuanza kwa tafiti hizo nne muhimu za kitaifa zitakazokusanya taarifa za kina kuhusu shughuli za biashara, sekta isiyo rasmi, huduma za fedha kwa wafanyabiashara wadogo na uzalishaji viwandani, hatua inayolenga kuimarisha mipango ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
Kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura ya 351, Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS imepewa jukumu la kuratibu na kusimamia uzalishaji, uchakataji na usambazaji wa takwimu rasmi nchini.
Tafiti hizo ambazo tayari zimeshaanza ni Utafiti wa Kina wa Shughuli za Kibiashara, Utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi, Utafiti wa Huduma za Fedha kwa Wafanyabiashara Wadogo Sana, Wadogo na wa Kati – FINSCOPE MSMEs pamoja na Utafiti wa Uzalishaji Viwandani ambazo taarifa zake ndizo zitakazokusanywa uwandani.
Madhumuni ya tafiti hizo ni kukusanya taarifa muhimu kuhusu shughuli za biashara katika sekta rasmi na zisizo rasmi, ikiwemo uzalishaji viwandani, ajira, uwekezaji na mazingira ya biashara nchini ambapo amesema taarifa zitakazopatikana zitaisaidia Serikali pamoja na wadau wa sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na watafiti kubuni programu mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.