NBS Accessibility Tools
NBS Accessibility Tools

Text Size

Language

Inflation Rate for September, 2026: 4.3% AASS 2023/2024 Women's Empowerment and Nutrition Module: WEN Tanzania Gender and Environment Survey: TGES 2025 Utafiti wa Kufuatilia Kaya (National Panel Survey, Wave 6: NPS 2026
The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Vijana Wenye Umri wa Miaka 15 hadi 35 Wanaunda 34.5% ya Watanzania Wote
Posted On: 12 October, 2026
Vijana Wenye Umri wa Miaka 15 hadi 35 Wanaunda 34.5% ya Watanzania Wote

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 wanaunda asilimia 34.5 ya Watanzania wote, ambapo amesema kuna umuhimu wa kuwekeza katika elimu, ujuzi, ajira na mitaji ili kuliwezesha kundi hilo kuchangia maendeleo ya taifa.

Prof. Mkenda ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Sumbawanga, mkoani Rukwa, ambapo amefafanua kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Tanzania ilikuwa na vijana zaidi ya milioni 21 wenye umri huo.

Kiongozi huyo amesema kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana kimepungua kutoka asilimia 8.3 mwaka 2024 hadi asilimia 7.5 mwaka 2025, lakini bado kuna haja ya kuongeza nafasi za ajira, ili kuimarisha ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kuweka mazingira bora ya kuwawezesha vijana kujiajiri wenyewe na kukuza biashara zao mbalimbali.

Kutokana na kaulimbiu ya Kongamano hilo isemayo, “Mazingira tofauti, fursa sawa kwa vijana,” Prof. Mkenda imesisitiza umuhimu wa kuhakikisha vijana wanapata fursa sawa za elimu, mafunzo, mitaji, masoko na teknolojia bila kujali maeneo wanayoishi au mazingira yao.

Prof. Mkenda amesema Wiki ya Vijana Kitaifa ni jukwaa la kuwaunganisha vijana, Serikali na wadau mbalimbali ili kujadili changamoto, kutambua fursa na kuweka mikakati ya kuongeza mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa.

Katika hatua nyingine, akiwasilisha mada kuhusu Takwimu za Vijana na Mchango wao katika Uchumi wa Taifa Kuelekea Dira 2050 tarehe 11 Oktoba 2026 katika Ukumbi wa Nazareti, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Mtakwimu Mwandamizi Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, Saruni Njipay amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya vijana nchini ni milioni 21.3 na inakadiriwa kufikia milioni 23.8 mwaka 2026.

Njipay amesema shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa na vijana na mchango wake katika uchumi wa nchi ambapo asilimia 45.0 ya vijana wanajishughulisha na kilimo, huku sekta hiyo ikichangia asilimia 54.4 ya ajira zote nchini kwa Mwaka 2025.

Pia, Njipay amefafanua kuwa kwa mujibu wa takwimu, nguvu kazi ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 imeendelea kuongezeka kutoka asilimia 70.6 mwaka 2024 na kufikia asilimia 73.1 kwa mwaka 2025 kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na uchumi wa Taifa ambao umeendelea kukua kwa asilimia 5.9 kwa mwaka 2025 ikilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka 2024 hivyo, amesema kundi la vijana ni muhimu katika uzalishaji, ubunifu na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

Mtakwimu huyo amehitimisha kwa kutoa wito kwa wadau, watumiaji na wazalishaji wengine wa Takwimu kutembelea Tovuti ya NBS na Maktaba Mtandao ya NBS (e-Library) ili kupata Takwimu Rasmi ambazo zitasaidia kupanga mipango mbalimbali.

NBS inazikaribisha taasisi, wadau na wananchi wa Mkoa wa Rukwa pamoja na maeneo jirani kutembelea Banda Namba 39 lililopo kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Ndua Manispaa ya Sumbawanga.