Wananchi, Wadau Wahimizwa Matumizi ya Takwimu Rasmi Utekelezaji Dira 2050
Kaimu Mkurugenzi wa Uratibu, Takwimu na Ubunifu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, James Mbogo, amewataka Wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kutumia Takwimu rasmi kwani ni misingi muhimu katika utekelezaji na kufikia malengo ya DIRA 2050.
Akizungumza katika Kipindi cha Joto la Asubuhi kupitia Kituo cha Redio cha Efm Mbezi Beach jijini Dar es Salaam leo tarehe 24 Septemba 2026, Mbongo amesema kupitia Takwimu rasmi, Tanzania inaweza kujenga uchumi jumuishi, shindani na wa kisasa unaotegemea viwanda, teknolojia, ubunifu, kilimo cha kisasa na sekta ya huduma kufikia mwaka 2050 na kufikisha wastani wa kipato cha mtu mmoja ukifikia angalau shilingi milioni 18 kwa mwaka, sawa na takribani shilingi milioni 1.5 kwa mwezi.
Mbongo ameongeza kuwa takwimu za Mfumuko wa Bei kwa Mwezi Agosti 2026 ulikuwa 4.3% ambao ni himilivu kwa nchi na kuweza kufikia malengo ya nchi kiuchumi hususan katika utekelezaji wa DIRA 2050.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Idara ya Ajira na Bei wa Ofisi hiyo, Hashimu Njowele ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wadadisi ili kuiwezesha NBS kupata taarifa zenye ubora ili kuzalisha Takwimu rasmi zitakazotumiwa na Serikali pamoja na wadau kuchochea maendeleo ya nchi.
Aidha, Wananchi na wadau wanaweza kupata Takwimu rasmi kupitia Tovuti ya NBS (www.nbs.go.tz) au kwenye kurasa za mitandao ya jamii ya NBS hususan Instagram na Facebook.