Sensa ya Watu na Makazi
Sensa ya Watu na Makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchakata, kuchambua, kutathmini, kuchapisha, kusambaza na kutunza takwimu za kidemografia, kiuchumi, na mazingira wanayoishi katika nchi kwa kipindi maalum. Zoezi la Sensa linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu SURA 351 na kwa kuzingatia Mapendekezo ya Umoja wa Mataifa yanayoitaka nchi mwanachama kufanya Sensa angalau mara moja ndani ya kipindi cha miaka 10. Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi yanasaidia kuongeza uwazi katika kugawa rasilimali zilizopo kuendana na uwiano wa idadi ya watu katika ngazi zote za utawala. Halikadhalika Matokeo ya sensa utumika katika kufuatilia na kutathmini mipango mbalimbali ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa, ikijumuisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2021/22 - 2025/26, Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (2021/22 - 2025/26), Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2050, Dira ya Maendeleo ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2050 na Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063.